‘Nitapona kweli leo?’ Huu ni mfano wa baadhi ya maswali yaliyokuwa yanayosumbua akili yangu kwa wakati huo. Nilikosa majibu ya maswali yangu, nikaishia kujisemea Mungu yupo.
Sasa endelea....
Tetemeko lilikoma ghafla, pakawa shwari tena, lakini giza lilikuwa lipo palepale. Mvua kubwa ilianza kunyesha, mwanga na miungurumo ya radi nilizidi kuvishuhudia.
Nilibaki nimeduwaa baada ya kugundua kuwa pale nilipokuwa silowi licha ya mvua kubwa kuendelea kunyesha. Hakuna hata tone moja la maji lililokuwa likinifikia utadhani nilikuwa chini ya mwamvuli, nilizidi kuchanganyikiwa.
Hata kwa chini maji hayakunigusa hivyo nyayo zangu zilikuwa kavu. Lakini mvua nilikuwa naishuhudia ikinyesha, tena ni bonge la mvua.
Nilibaini kuwa kumbe nilikuwa nipo juu ya kilima baada ya mwanga wa radi kumulika. Lakini hapakuwa hata na mwamvuli juu yangu licha ya kutoangukiwa na tone hata moja.
Mara niliona kitu kama shuka jeupe kikishuka kutoka angani. Nilikisubiri kwa hamu kitu hicho ili nione ni nini kitatokea.
Woga ulianza kupungua. Siyo kwa kuwa nilikuwa nimeyazoea mazingira; la hasha! Ulipungua kutokana na kukata tamaa nikijua kuwa kuokoka kwangu ni asilimia 0.0025. Nilijipa uhakika wa kupoteza uhai endapo kudura za Mwenyezi Mungu zisingechukua nafasi.
Kitu hicho kilizidi kuteremka taratibu, tena kilikuwa wima mithili ya kitambaa cha sinema. Japokuwa giza lilikuwa limetanda angani kote, kitu hicho kiling’ara na niliweza kuushuhudia mng’ao wake. Shauku ya kutaka kuona kitakachotokea ilizidi kunishika, moyo wa woga haukuwepo tena kwa wakati huo.
Kitu hicho kilianguka chini, moshi mwingi niliushuhudia kilipokuwa kimeangukia. Moshi uliendelea kutoka mahali hapo lakini kitu hicho mfano wa shuka kilikuwa hakionekani tena.
Kufumba na kufumbua niliwaona watu katikati ya moshi huo, nikashindwa kujua idadi yao kamili kwa sababu walikuwa wanatembeatembea bila ya kutulia. Licha ya moshi mwingi kutanda eneo hilo, watu hawa walionekana ‘live’ tena bila chenga.
Nilizidi kuchanganyikiwa nilipoanza kuwatambua baadhi yao, kilichokuwa kinanishangaza ni kwamba kila niliyemtambua alikuwa kashatangulia mbele ya haki tukamzika, yaani namaanisha alishakufa kitambo.
Itaendelea......
No comments:
Post a Comment